Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (AS) – ABNA – Redio ya jeshi la utawala wa Kizayuni imetangaza kuuawa kwa wanajeshi saba kutoka kikosi cha 605 cha uhandisi wa kivita cha jeshi hilo huko Ukanda wa Gaza, baada ya gari la kubeba askari la kivita lililokuwa limewabeba kulengwa na vikosi vya muqawama wa Palestina mashariki mwa mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa Israel, mlipuko huo ulitokea jana jioni majira ya saa 17:30, wakati mmoja wa wapiganaji wa Palestina alipokaribia gari hilo la kubeba askari na kuweka bomu lililotengenezwa kwa mkono. Mlipuko wa bomu hilo ulisababisha moto kuwaka ndani ya gari hilo, na gari hilo liliteketea kabisa.
Jeshi la utawala wa Kizayuni limetangaza kuwa vikosi vya zimamoto vya kijeshi vilifika eneo hilo na kufanya jitihada kubwa za kudhibiti moto. Walitumia hata tingatinga la kijeshi aina ya D-9 kumwaga mchanga juu ya gari hilo, lakini jitihada zote hazikufanikiwa.
Kulingana na maelekezo ya uwanjani, iliamuliwa kuwa gari hilo lipelekwe ndani ya ardhi zinazokaliwa, kupitia barabara ya Salahuddin, huku wanajeshi wote saba wakiwa bado ndani yake.
Baada ya kufika ndani ya maeneo yanayokaliwa ya Palestina, vikosi vya zimamoto hatimaye vilifanikiwa kuzima moto, lakini wanajeshi wote walikuwa wameuawa.
Redio ya jeshi la utawala wa Kizayuni imethibitisha kuwa operesheni ya kutambua utambulisho wa waliokufa ilichukua masaa mengi na familia zao zilifahamishwa kuhusu suala hilo jana usiku.
Your Comment